HALI ya mgombea ubunge katika jimbo la Bukombe mkoani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Bw. Emmanuel Luhahula imeelezwa kuwa bado ni tete na nguvu za ziada zinahitajika ili kumuwezesha kuibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.



Hali hiyo inatokana na wanachama wa Chama cha mapinduzi (CCM) katika jimbo hilo kutoridhishwa na uteuzi wa Bw. Luhahula uliofanywa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC) ambapo hivi karibuni mgombea huyo alikataliwa na kuzomewa mbele ya Rais Jakaya Kikwete.



Kutokana na upepo kuwa mbaya Chama cha Mapinduzi kimewapeleka katibu mkuu wake, Bw. Yusuf Makamba pamoja na kada wake mwingine, Bw. Raphael Chegeni ambaye ni mjumbe wa kitaifa wa uratibu wa kampeni za CCM ili kujaribu kurekebisha hali ya hewa katika jimbo hilo.



Hata hivyo pamoja na ujio wa viongozi hao wakuu bado hali si shwari ambapo baadhi ya wanachama waliozungumza na Majira kwa njia ya simu jana wamekiomba chama hicho kumpeleka Bw. Samuel Malecela maarufu kama ‘tingatinga’ ambaye wanaamini mbinu zake zinaweza kurekebisha mchafuko wa hewa ndani ya CCM katika jimbo hilo.



“Kwa kweli hali bado ni ngumu kwa mgombea wetu wa CCM, watu wengi wanaelekea kumuunga mkono mgombea wa CHADEMA, Profesa Kulikoyela Kahigi, huyu huenda akaibuka na ushindi mkubwa iwapo CCM isipojipanga vizuri,” alieleza Bw. Said Malingumu, mkazi wa Ushirombo.



Bw. Malingumu alisema tatizo la kukataliwa kwa Bw. Luhahula linachangiwa na viongozi wenyewe wa CCM ambao baadhi yao walishinikiza kuteuliwa kwake pamoja na kwamba walielewa fika hakubaliki kwa wakazi wa Bukombe.



Mmoja wa wana CCM ambaye hakupenda kutajwa gazetini alisema chanzo cha vurugu na kukataliwa kwa mgombea wao kinachangiwa na kamati ya siasa ya wilaya hiyo ambayo pamoja na kupelekewa vielelezo vikionesha mapungufu ya Bw. Luhahula, lakini bado walipendekeza kuteuliwa kwa jina lake.



“Unajua wanachama kama wanachama hawana tatizo, chanzo cha yote haya ni kamati ya siasa ya wilaya, hawa ndiyo waliopendekeza jina la Bw. Luhahula, wengi walijali maslahi yao wakasahau maslahi ya umma, sasa hali ni ngumu kwa kweli, juhudi zinahitajika kulinusuru jimbo lisiende upinzani,”



“Wamekuja hapa Bw. Makamba (Yussuf) na Bw. Chegeni, lakini tunaona kama vile wanazidi kuvuruga mambo, tunafikiri angekuja Bw. Malecela anaweza akaweka mambo sawa, maana huyu ni mzoefu, tulimuona kule Solwa, Bariadi Mashariki na Kishapu katika chaguzi ndogo zilizopita, alimudu mambo,” alieleza mwanachama huyo.



Hata hivyo kwa upande mwingine mmoja wa viongozi waandamizi ndani ya CCM (Jina tunalo) alimlaumu mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Bw. Hamisi Mgeja kuwa ndiye aliyechangia kwa kiasi kikubwa mpasuko katika jimbo hilo .



Alisema Bw. Mgeja katika uteuzi wa wagombea yeye binafsi alikuwa na mtu wake (hakumtaja) ambaye hata hivyo hakuteuliwa hali ambayo imekuwa chanzo cha kukataliwa kwa mgombea aliyeteuliwa na chama (Bw. Luhahula).



“Kwa kweli hata kiongozi wetu wa mkoa huyu mwenyekiti Mgeja amechangia tatizo, nafikiri alikuwa na mtu wake, sasa alipoona huyo aliyemtaka yeye hakuteuliwa basi amekuwa na kinyongo na mgombea aliyeteuliwa japo hajioneshi rasmi.



Aidha kwa upande mwingine wanachama hao wanahusisha uhamisho wa ghafla uliofanyika hivi karibuni wa katibu wa CCM wilayani Bukombe, Bw. Mberito Magova kuwa unatokana na mvutano ulioanza katika kipindi cha upigaji wa kura za maoni ndani ya CCM ambapo katibu huyo alisimamishwa kwa muda na uongozi wa mkoa.



Akizungumza kwa njia ya simu na Majira, Bw. Magova alikiri kupewa uhamisho huo na kwamba ametakiwa kuripoti makao makuu ya Chama mkoani Dodoma ambako atapangiwa kazi nyingine.



“Ni kweli nimepata uhamisho, na hivi ninavyoongea na wewe tayari nimeishakabidhi shughuli zote za ofisi kwa katibu mpya aliyeletwa na mimi najipanga kesho (leo) kuelekea Dodoma kuripoti, japo sifahamu nitakuwa katika nafasi gani maana sijaelezwa,” alieleza Bw. Magova.



Hata hivyo katibu huyo hakuweza kueleza kwa kina sababu ya uhamisho huo wa ghafla japo alikiri kuwepo kwa mtafaruku kati yake na baadhi ya viongozi wa mkoa ambao alidai walipeleka taarifa za uongo dhidi yake kwa katibu mkuu wakati wa zoezi la upigaji wa kura za maoni ndani ya CCM.



Kwa upande wake Bw. Mgeja alipinga tuhuma za yeye kuwa na mtu wake ambapo alisema wanachama wote kwake wana haki sawa, na kwamba wanaoeneza uvumi huo hawakitakii kheri chama chake na wana ajenda yao ya siri.



“Hizo ni fitina na majungu tu, mimi sikuwa na mtu ye yote aliyekuwa chaguo langu, wana CCM wote ni wangu, na hivi sasa tunapigana kufa na kupona kumnadi mgombea aliyeteuliwa na Chama ili aweze kupata ushindi na si vinginevyo,” alieleza Bw. Mgeja.



Alisema anavyofahamu yeye hakuna mpasuko wowote ndani ya CCM mkoani Shinyanga na kwamba hivi sasa wapo katika harakati za kuwanadi wagombea wote wa CCM akiwemo Bw. Luhahula mwenyewe ili waweze kuibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao.



Hivi karibuni wakati mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete alipotembelea wilayani Bukombe ikiwa ni katika kampeni za kuomba kura kutoka kwa wananchi, umati wa wakazi wa mjini Ushirombo ulimkataa na kumzomea Bw. Luhahula baada ya kunadiwa na Rais Kikwete.



Mwisho.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top