Namtumbo, Ruvuma

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amekanusha kauli zilizotolewa na baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani wanaodai vyandarua vinavyosambazwa na serikali vinatokana na fedha za mauzo ya madini ya Uranium.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wakazi wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma katika moja ya mikutano yake ya kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika jana mjini Namtumbo.

Rais Kikwete akionesha kukerwa na kauli hizo alisema mpaka hivi sasa hakuna madini yoyote ya Uranium yaliyoanza kuchimbwa hapa nchini na kwamba kazi inayofanyika bado ni ya utafiti na siyo uchimbaji.

Alisema wapinzani wamekosa cha kuwaeleza watanzania na badala yake wanatafuta kila mbinu zitakazowawezesha kuwafikisha Ikulu hata kama ni kwa kuwadanganya wananchi kitu ambacho alikikemea vikali.

“Ndugu zangu wamepita hapa hawa wenzetu wa vyama vya upinzani, wamesema uongo kuwa eti hivi vyandarua vinavyotolewa bure na serikali vinatokana na fedha ya mauzo ya madini ya Uranium, siyo kweli huu ni uongo, haya madini hayajaanza kuchimbwa hapa nchini,”

“Kinachofanyika hivi sasa ni utafiti na utafiti huu unatarajiwa kukamilika mwaka 2012, na kama ni kuanza uzalishaji basi utaanza baadae kabisa na mimi hapa nitakuwa nimemaliza kipindi changu cha urais, nafikiri wenzetu wamekosa ya kusema, lakini kama mtu umekosa la kusema ni vizuri ukanyamaza, badala ya kutunga uongo,”

“Nilikuwa sipendi kuwazungumza hawa watu, nilijitahidi sana kuzungumzia mambo yetu na yale ambayo chama chetu kimeyatekeleza katika kipindi kilichopita, lakini hawa wenzetu sasa wamezidi uongo, wanatafuta uongozi kwa gharama yoyote ile, hapana huu ni uongo wa mchana,” alieleza Rais Kikwete.

Rais Kikwete aliwaomba wakazi wa wilaya ya Namtumbo kuwa ili wathibitishe maelezo yake ni vizuri wakateua wajumbe ili waende wenyewe katika eneo linalofanyiwa utafiti wa kuwepo kwa madini hayo huko katika kijiji cha Lukuyu ambako utafiti unafanyika ili waweze kujionea ukweli kwa vile alichokieleza si cha kujipigia debe.

“Nayasema haya siyo kwamba najipigia debe, uranium haijaanza kuuzwa na serikali hivi sasa ndiyo kwanza imeanza kutengeneza muongozo wa jinsi itakavyoshirikiana na wawekezaji katika kuendesha machimbo hayo iwapo madini yatapatikana, yarabi toba, hapa sijipigii debe, nakuombeni teueni wajumbe waende wakathibitishe,” alieleza.

Kwa upande mwingine Rais Kikwete alitoa ufafanuzi kuhusiana na safari zake za mara kwa mara za nje ya nchi ambapo alisema safari hizo zimekuwa na manufaa makubwa kwa nchi kinyume na inavyodaiwa na wapinzani kuwa amezidi kusafiri sana.

“Jamani hivi kweli nikikaa pale Ikulu muda wote tunaangaliana na mama Salma Kikwete haya mafanikio tuliyoyapata yasingekuwepo leo hii, safari zangu za nchi za Japan na Marekani zimetuwezesha tupate msaada uliosaidia ujenzi wa barabara zetu nyingi nchini kwa kiwango cha lami, ningekaa tu zisingepatikana,” alieleza Rais Kikwete.

Pia Rais Kikwete alitahadharisha suala la kuchagua viongozi kwa kuzingatia misingi ya kidini na kwamba katika siasa watu hawashindanishi vitabu vya Qur-an na Biblia isipokuwa kinachoshindanishwa ni Sera za chama husika na kuelezea jinsi gani chama kitafanya katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Akizungumza utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, Rais Kikwete alisema mambo mengi yaliyoahidiwa na chama chake yametekelezwa na yale ambayo hayajatekelezwa yako mbioni kukamilishwa.

Aliwataka wananchi waendelee kukichagua Chama cha Mapinduzi kwa vile ndicho pekee chenye kutoa ahadi na kuzitekeleza kinyume na vyama vingine, ambapo aliwataka wananchi wawe wakiwahoji ni mambo yapi ya maendeleo ambayo wameishawatekelezea.

Aidha alisema hivi sasa serikali imeanza mchakato wa kuupatia nishati ya umeme mji wa Namtumbo baada ya kununua jenereta kubwa ya kuzalisha umeme ambayo hivi karibuni itawasili nchini na kufungwa katika mji huo wa Namtumba.

Hata hivyo alisema pamoja na kununuliwa kwa jenereta hiyo mipango imo mbioni ya kuhakikisha mkoa wa Ruvuma unapatiwa umeme kutoka katika gridi ya Taifa ambapo utakapofika Songea pia utapelekwa katika mji wa Namtumbo.

Kuhusu suala la afya, Rais Kikwete alisema serikali itasaidia ukarabati wa kituo cha afya cha Namtumbo ambacho imeamriwa kipandishwe hadhi ya kuwa hospitali ya wilaya na kwamba tayari serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya kazi hiyo.

Pia alisema katika kuimarisha miundo mbinu ya barabara tayari kazi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami imeanza kutoka Namtumbo hadi Tunduru na Namtumbo – Songea hadi Mbinga na kwamba barabara hizo zitakapokamilika zitarahisisha mawasiliano ya wakazi wa mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine nchini pamoja na kuinua kipato cha wananchi wake.

Rais Kikwete jana alifanya mikutano ya kampeni katika miji ya Namtumbo, Matemanga na Tunduru mkoani Ruvuma na leo inatarajiwa kuendelea na mikutano hiyo mkoani Mtwara.

Mwisho.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top