Siku nne baada
ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwahukumu kifungo cha miaka mitatu jela
mawaziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Daniel Yona na Basil
Mramba, upande wa mashitaka umewasilisha kusudio la kukata rufaa.
Kwa mujibu wa
kusudio hilo lililowasilishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
wanapinga adhabu na hukumu iliyotolewa na jopo la mahakimu watatu, John Utamwa,
Sam Rumanyika na Saul Kinemela, pamoja na kuachiwa huru kwa aliyekuwa Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Hakimu mfawidhi
wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha alisema kusudio hilo limeshawasilishwa na
upande wa mashitaka mahakamani hapo.
Wakati upande
wa mashitaka ukichukua hatua hiyo, mawakili wa kina Mramba na Yona nao wameanza
mchakato wa kutaka ‘kuwachomoa’ gerezani na kuwarudisha uraiani kwa kuomba
wapatiwe dhamana wakati watakapokuwa wakisubiri rufaa yao kusikilizwa.
Mramba na Yona
walihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kifungo cha miaka mitatu jela
baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na
kuisababishia hasara serikali ya Sh11.5 bilioni.
Hata hivyo,
wakili wa Yona, Elisa Msuya, juzi alisema kwasasa wanaandaa maombi ya dhamana
na wakati wowote watafungua maombi hayo Mahakama Kuu ya Dar es Salaam, wakati
wakisubiri kukata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa.
Akizungumzia
azma hiyo, Wakili wa Serikali, Charles Anindo alisema kwa mujibu wa
kifungu cha 368 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai sura ya 20
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009, kinaruhusu mfungwa kuombewa dhamana
wakati rufaa yake inasubiri kusikilizwa.
Hata hivyo,
Wakili Anindo alibainisha kuwa kifungu hicho kinahusika tu kama kuna uwezekano
mkubwa wa rufaa hiyo kushinda.
Hata hivyo,
wakati Yona na Mramba wakitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo hicho, Mgonja
aliachiwa huru baada ya mahakama kuridhika kuwa hana hatia kwa mashitaka kumi
na moja yaliyokuwa yakimkabili.
Akisoma hukumu
hiyo kwa niaba ya jopo la mahakimu watatu waliokuwa wakiisikiliza kesi
hiyo, Hakimu Mkazi, Sam Rumanyika alisema baada ya kupitia ushahidi
uliotolewa na mashahidi 13 wa upande wa mashitaka na mashahidi sita wa upande
wa utetezi wakiwamo washitakiwa wenyewe, walimuachia huru Katibu Mkuu wa zamani
wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja kwa kuwa upande wa mashitaka ulishindwa
kuthibitisha mashitaka yake pasi kuacha shaka.
Mramba alitiwa
hatiani katika mashtaka yote kumi na moja yaliyokuwa yakimkabili na katika
shitaka la kwanza hadi la 10 ambayo ni ya matumizi mabaya ya madaraka na
kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila shitaka.
Hata hivyo,
watatumia miaka mitatu tu kwani adhabu zote zinakwenda sambamba.
Katika
shitaka la kumi na moja ambalo ni la kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7
bilioni alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela ama kulipa
fidia ya Sh5 milioni.
Yona
alitiwa hatiani kwa mashitaka manne, shtaka la kwanza, la pili, la tatu na la
tano ambayo ni ya matumizi mabaya ya madaraka pamoja na la kumi na moja la
kuisababishia hasara Serikali ya Sh11.7 bilioni.
Chanzo: Mwananchi
News
Post a Comment