Ni dhahiri kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeingiwa hofu inayokifanya kishindwe kutangaza mchakato na ratiba za vikao vya uteuzi wa wagombea wake wakiwamo wa urais na ubunge katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu, NIPASHE imeelezwa. 
 
Kufikiwa kwa hatua kama hiyo kwa vyama vikubwa vya upinzani nchini, kunaifanya CCM ibaki njia panda, hali iliyo tofauti na nyakati kama hizi katika kuelekea chaguzi zilizofanyika hususani zikihusisha vyama vingi tangu kuanzia 1995.
 
Taarifa za uhakika zilizothibitishwa na vyanzo tofauti ndani ya CCM (majina tunayahifadhi) zilieleza kuwa, hali ilivyo mwaka huu kwa chama hicho inachangiwa na sababu tofauti, ikiwamo mkakati wa `kuwatosa’ wagombea wasiokubalika kwa baadhi ya viongozi na `kuwabeba’ wasiokuwa na mvuto kwa wapiga kura.
 
“Hali hii inawafanya (viongozi) washindwe kutimiza wajibu wao katika kutoa ratiba na kutangaza mchakato wenye kutoa taarifa na uhuru kwa wanachama wake kuchukua fomu za uteuzi,” kilieleza chanzo chetu.
 
Tangu mwaka 1995, CCM imekuwa ikitangaza mchakato na ratiba za kura za maoni na kuwapata wagombea kabla ya vyama vya upinzani, hali iliyovifanya  vyama vya upinzani kutoa fursa kwa baadhi ya walioshindwa katika kura za maoni (za CCM) kugombea nafasi tofauti kupitia vyama hivyo.
 

Jitihada za NIPASHE kumpata Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, kuzungumzia hali hiyo hazikuzaa matunda jana kwani simu zao hazikuwa hewani.
 
Hata hivyo, Ofisa mmoja katika ofisi ndogo za chama hicho, Lumumba jijini Dar es Salaam, alisema kuchelewa kwa mchakato na ratiba hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mfumo wa utendaji kazi ndani ya CCM.
 
Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa vile si msemaji rasmi wa CCM, alisema kimsingi mgombea urais kupitia CCM alipaswa kufahamika jana na leo angetangazwa rasmi kwa umma.
 
Kwa mujibu wa ofisa huyo, CCM haijutii pale vyama vya upinzani vinapotangaza ratiba na mchakato wa kura za maoni kabla yake (CCM).
 
“Kwa vile sisi tulikuwa na utaratibu wa kuanza kabla yao (wapinzani) na sasa tupo katika utendaji wa kawaida, wao wanapotangaza kabla yetu (CCM) linakuwa jambo jipya, lakini kila taasisi ina mfumo wa utendaji kazi wake,“ alisema.
 
Ofisa huyo alisema CCM imefanya mageuzi makubwa katika mfumo wa uteuzi wa wagombea wake mwaka huu ikiwamo kwa nafasi ya urais.
 
Bila kutaka kuingia kwa undani, alisema mageuzi hayo yanayoweza kuwa na changamoto zake.
 
Tayari kumekuwa na mapendekezo kadhaa juu ya mfumo unaofaa wa kura ya maoni ndani ya CCM hasa kuhusu nafasi za ubunge.
 
Wakati wa Mkutano wa Bunge uliopita, wabunge wa CCM walijadili pamoja na mambo mengine, mapandekezo mapya ya mfumo wa kura ya maoni wa kuwa na wagombea watatu tu watakaopigiwa kura na mkutano mkuu wa jimbo baada ya majina ya waombaji wote kuchujwa na chama ngazi husika.
 
Kadhalika, kulikuwa na pendekezo la kutaka wabunge ambao wamethibitika kutekeleza ilani ya CCM kwa ufanisi unaotosheleza, wasiwe na wapinzani ndani ya chama na wapitishwe kuwania tena nafasi hizo kama bado wanataka kugombea.
 
Mikakati hii mipya inaelezwa kuwa inachukuliwa na CCM ili pamoja na mambo mengine, kuzuia uwezekano wa kupoteza majimbo kwa sababu tu ya watu kutoridhishwa na matokeo ya kura ya maoni, hali ambayo kwa miaka mingi imesababisha walionyanganywa ushindi kuhamia upinzani na kushinda.
 
Pia inachukuliwa kama tiba ya kukabiliana na matumizi ya fedha (rushwa) katika uchaguzi huo.
 
Hata hivyo, kuna taarifa kwamba CCM inavuta pumzi kutoa ratiba kamili ya uteuzi wa wagombea ili kuondoa kila uwezekano kwa wale watakaoshindwa au kuwekewa mizengwe kwenye nafasi ya urais kukimbilia upinzani.
 
“Sikiliza rafiki yangu, wewe unafikiri kwa hali ilivyo sasa hivi ni rahisi tu kuanza kuweka kila kitu wazi mapema? Tunataka kuwa na muda mfupi wa mchakato ili kupunguza madhara kwa chama. Tunataka tuingie kwenye uchaguzi mkuu tukiwa wamoja siyo vipande vipande,” alisema kada wa CCM makao makuu.  

Source: NIPASHE
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top