RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - JAKAYA MRISHO KIKWETE. |
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe (kulia) akiteta jambo na mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete. |
UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umemtaka Rais Jakaya Kikwete,
ahakikishe anamaliza muda wake wa uongozi salama pasipo kuiacha nchi kwenye
machafuko kwa kushinikiza upatikanaji wa Katiba Mpya na matumizi ya mfumo mpya
wa uandikishaji wapigakura kwa njia ya kielektroniki (BVR), wakati hakuna
maandalizi ya kutosha.
Viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD,
walitoa tamko hilo wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam wakielezea athari zinazoweza kutokea kutokana na Serikali ya Rais
Kikwete,kushinikiza matumizi ya BVR na kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa.
Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe, alisema kutokana na hali inavyozidi
kuwa mbaya ni wazi kwamba shinikizo la kulazimisha wananchi kuandikishwa kwa
mfumo wa BVR, linaweza kuiacha nchi kwenye machafuko.
Alisema shinikizo hilo linatokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani chama
hicho, ndicho kinanufaika na BVR; na kwamba UKAWA tayari ilishaweka msimamo wa
kutoshiriki kupiga kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa.
"Ili Rais Kikwete aiache nchi katika amani yake na kuepuka machafuko
ni vyema aache kushinikiza masuala hayo, asubiri amalize muda wake wa miaka 10
kuliko kuendelea kushinikiza wananchi kutumia BVR huku wananchi wengine wakiwa
hawana taarifa na nini kinachoendelea kuhusiana na uandikishwaji kwa kutumia
mfumo huo," alisema Mbowe.
Alisisitiza kwamba lazima ieleweke kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
haina fedha, lakini pia Sheria inahitaji NEC kuboresha Daftari la Kudumu la
Wapigakura angalau mara mbili kabla ya Uchaguzi Mkuu mwingine unaofuata.
"Lakini kwa makusudi Serikali ya Rais Kikwete imevunja sheria ya
kuboresha daftari hilo," alisema na kuongeza;
"Kitendo hiki kina malengo mabaya ya kutaka kuongeza muda wa utawala
wake kwa kisingizio kuwa Uchaguzi Mkuu hauwezi kufanyika kwa datari hilo ambalo
halijaboreshwa," alisema Mbowe.
Naye Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema juzi uongozi wa
UKAWA ulipata taarifa kuhusiana na hali inayoendelea Makambako, mkoani Njombe
ambako uandikishaji wa majaribio unafanyika.
Alisema katika uandikishaji huo wa majaribio mifumo ya BVR imeshindwa
kufanya kazi hali inayochangiwa kutokuwepo kwa maandalizi kwa watendaji wake.
"Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali kutoka kwa viongozi wetu walioko
eneo la uandikishaji wa wapigakura, mfumo huo ulifeli kabla ya kuzinduliwa
rasmi juzi na Waziri Mkuu na kupigiwa chapuo na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi," alisema Prof. Lipumba.
Alitaja maeneo ambako mfumo huo umeonesha kufeli kuwa ni NEC kutokuwa na
watumishi wa kufanya kazi hiyo na kupuuza ushauri wa mwelekezi kutoka Marekani.
Alisema mtaalamu huyo alishauri NEC iwe na watumishi zaidi 10,000 kwa
ajili ya kufanikisha uandikishaji huo nchi nzima,lakini
haikufanyika hivyo.
Lakini pia alisema watumishi wa NEC walioanza kufanya kazi mkoani Njombe
wamepatiwa elimu kwa muda wa siku moja tu kabla ya zoezi hilo kuanza na huku
wengine wakiwa hawajui hata kushika kamera.
Alisema matatizo yaliyojitokeza katika zoezi la uandikishaji wapigakura
yanaonesha wazi kuwa Daftari la Wapigakura halitakamilika ili litumiwe katika
zoezi la kura ya maoni.
"Ni vyema Rais Kikwete akakubali ukweli huu. Suala la kura ya maoni
liahirishwe mpaka baada ya uchaguzi," alisema na kuongeza; " Tatizo
kubwa zaidi ni kuwa Tume kushindwa kuandikisha wapigakura wote kabla ya
Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa sababu mashine za kuandikisha wapigakura zina
hitilafu."
Source: Majira News
Post a Comment