KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wakazi wa kata ya
Masekelo manispaa ya Shinyanga juzi walilazimika kususia mazishi ya mmoja wa
wakazi wa kata hiyo baada ya wana ndugu kushinikiza kufanya vitendo vya kimila
makaburini ikiwemo kuupasua mwili wa marehemu kabla ya kuzikwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, kitendo cha
wanandugu wa marehemu aliyetajwa kwa jina la Bernadetha Stephen (35) aliyekuwa
akiishi mtaa wa Mapinduzi katika kata hiyo ya Masekelo kushinikiza kumpasua
marehemu kabla ya mazishi kilisababisha kutokea kwa vurugu kubwa eneo la
makaburini.
Hata hivyo awali siku moja kabla ya kuzikwa kwa
marehemu huyo baadhi ya wanandugu walitishia kususia kumzika ndugu yao kutokana
na kitendo cha mumewe kushindwa kumlipia mahari hali na hivyo kushinikiza
walipwe kwanza kiasi cha shilingi milioni moja ndipo washiriki mazishi.
Mashuhuda hao walisema kutokana na msimamo wa
wanandugu kulazimisha kutekeleza mambo yao ya kimila sehemu kubwa ya wananchi
iliamua kususia mazishi hayo na kuondoka katika eneo la makaburi na kuwaacha
wakiendelea kutekeleza mila zao za kikurya.
Wakifafanua walisema marehemu Bernadetha alifariki
dunia Januari mosi mwaka huu akiwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga
akipatiwa matibabu kutokana na kusumbuliwa kwa ugonjwa wa tumbo unaohisiwa kuwa
chanzo cha kifo chake ambapo mazishi yake yalifanyika juzi mchana huko katika
makaburi ya kata ya Masekelo.
Walisema marehemu huyo alikuwa akisumbuliwa na uvimbe
tumboni ambapo ambapo mmoja wa ndugu aliyetokea mkoani Mara inadaiwa ndiye
aliyeshinikiza kufanyika kwa mambo hayo ya kimila kwa lengo la kuondoa mikosi
ndani ya familia yao kutokana na wanandugu wengi kufariki dunia kwa ugonjwa
huo.
Hata hivyo wanajamii waliokuwa wamehudhuria katika
mazishi hayo walipinga vikali kitendo hicho na kushauri kuwa kama pangekuwa na
ulazima wa kutekeleza mila hiyo basi kazi hiyo ingefanyikia hospitali eneo
ambalo ni la faragha badala ya kulitekeleza mbele ya kadamnasi ya watu.
Mmoja wa mashuhuda hao (jina limehifadhiwa) alisema
mgogoro huo ulianzia nyumbani kwa marehemu kabla ya kuelekea makaburini ambapo
baadhi ya ndugu pamoja na kuielewa hali hiyo walionesha utulivu lakini baada ya
kufika makaburini na kuanza shughuli za mazishi ndipo mmoja wa wanandugu
alipoingia kaburini akiwa na wembe mkononi.
“Tulipokuwa nyumbani dalili za kutokea vurugu zilianza
kujionesha, lakini sehemu kubwa ya wanandugu walitulia mpaka pale tulipofika
eneo la makaburi na kuanza shughuli za mazishi, ghafla mmoja wana ndugu
aliingia kaburini akiwa ameshika wembe mkononi huku amevaa glovu,”
“Wakati akiingia kaburini alikuwa pia ameshika boksi
dogo ndani yake kukiwa na kifaranga cha kuku ambapo aliwazuia wananchi kuacha
mara moja shughuli ya kutupia udongo kaburini ambapo ghafla alifungua sanduku
lililokuwa limehifadhi mwili wa marehemu na kuanza kumchana tumbo lake kwa
wembe,” alieleza shuhuda huyo.
Alisema hali hiyo iliwashitua watu wengi ambao sehemu
kubwa waliamua kususia mazishi hayo na kuondoka katika eneo la makaburi ambapo
ndugu huyo alimchinja kuku aliyekuwa naye na damu yake aliimwaga kwenye mwili wa
marehemu na kisha kumwingiza kuku yule kwenye tumbo la marehemu kwa imani kwamba ni kumaliza mkosi ndani ya ukoo wao.
“Alipomaliza kumwingiza kuku yule katika tumbo la marehemu ndipo
alipofunika tena sanduku lile na yeye kutoka nje ya kaburi ambapo aliwaomba
wananchi waendelee na kazi ya ufukiaji wa kaburi lile hata hivyo sehemu kubwa ya wananchi
walikuwa wameisha ondoka katika maeneo hayo ya makaburi,” aliendelea kueleza shuhuda wa tukio hilo.
Akielezea tukio hilo Ofisa mtendaji kata ya Ndala, Dickson Venance alisema
kabla ya siku moja ya mazishi palitokea mgogoro kati ya aliyekuwa mume wa
marehemu ukihusiana na suala la mahari ambapo walishinikiza kupasua mwili wa
marehemu na kasha waondoke naokwenda kuzika kwao mkoani Mara.
“Nilijitahidi kusuluhisha mgogoro huo ambapo ndugu walikubali kulipwa kiasi
cha shilingi laki moja ambapo ndugu wa upande wa mume walichangishana na kufanikiwa
kupata kiasi hicho cha fedha na kuzikabidhi kwa ndugu wa marehemu walioridhia
mazishi hayo kufanyika mjini Shinyanga,” alieleza Venance.
Hata hivyo ilielezwa baadhi ya wananchi waliamua kutoa
taarifa za tukio hilo katika kituo cha polisi ambao walifikia katika eneo la
makaburi wakati shughuli za mazishi zikiendelea na kuwakamata wanandugu wote
waliohusika na uendeshaji wa shughuli kimila kinyume cha utaratibu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus
Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanandugu waliohusika
walikamatwa na kuhojiwa kwa muda na ilipobaika ni mambo ya kimila waliachiwa
huru na kuruhusiwa kuendelea na shughuli za mazishi.
Post a Comment