Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE, John Myola akitoa salamu zake za mwaka mpya wa 2015 kwa watoto wanaotunzwa na shirika hilo ambao wanachukua mafunzo mbalimbali ikiwemo stadi za maisha katika kituo cha Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Buhangija Manispaa ya Shinyanga.
Semeni basi je! tumependeza au hatujapendezaaaa!!!!? HAPPY NEW YEAR!!! - 2015. 
Hawa nao hawakuwa nyuma, wanaonekana wakiwa wametulia kwa umakini mkubwa wakifuatilia shamra shamra za kuadhimisha mwaka mpya wa 2015 zilizofanyika katika kituo cha FDC Buhangija Shinyanga.
Tunalipongeza Shirika la AGAPE kwa kutukumbuka pia sisi katika kusherehekea mwaka mpya wa 2015, kwa kweli tumefarijika na kujiona na sisi ni miongoni mwa jamii ya watanzania, ndivyo alivyoelezea furaha yake mmoja wa watoto wanaotunzwa na Agape.
Mmoja wa watoto wanaotunzwa na kupatiwa mafunzo ya ufundi stadi na AGAPE akionesha ujuzi wake kwa watoto wenzake wakati wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2015.
Mkurugenzi wa AGAPE, John Myola akimzawadia fedha mmoja wa watoto walioshiriki katika hafla ya kuukaribisha mwaka mpya baada ya kufurahishwa na show yake.
WATOTO wa kike waathirika wa mimba na ndoa za utotoni wanaotunzwa na Shirika la AGAPE mkoani Shinyanga wameshauriwa kutojinyanyapaa na kujiona wapweke kutokana na matatizo yaliyowapata na badala yake wajikite zaidi katika mafunzo wanayopatiwa na shirika hilo.
 
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la AGAPE, John Myola alipokuwa akitoa salaam zake za kuuaga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2015 kwa watoto hao ambapo aliwataka wamshukuru mungu aliyewawezesha kuingia salama katika mwaka mwingine wakiwa salama.
 
Myola alisema badala ya watoto hao kukaa wakijisikitikia kutokana na masahibu yaliyowapata ni muhimu wakatafakari na kumshukuru mungu aliyewawezesha waendelee kuishi wakati wapo wengine wengi waliokuwa wamejiandaa kwa mipango mizuri kuelekea mwaka huu wa 2015 lakini hata hivyo wameaga dunia kabla ya kuuona mwaka huu.
 
“Wakati tukiingia mwaka 2015 tusisikitike na kujiona wanyonge kwa masahibu yaliyotupata, badala yake tukae chini tutafakari ni vipi wenzetu wengine wameondoka na sisi tuendelee kuishi, tujiulize tumebaki kwa lipi? Je, ni kwa mabaya au kwa mazuri?, kama ni wabaya basi tujisahihishe kwa kuangalia matendo yetu ya nyuma ya mwaka uliopita,”
 
“Kama ni wazuri basi tuongeze juhudi zaidi katika utendaji wa shughuli zetu, na tuelewe kila mwaka mpya unapoanza ni kipindi kizuri cha kujipanga kuangalia mambo gani ya muhimu tutakayoyatekeleza katika mwaka huo, kwa upande wenu lazima  mjikite katika kutumia fursa hii ya kujifunza mafunzo mnayopatiwa hapa,” alieleza Myola.
 
Kwa upande mwingine Myola aliwataka watoto hao kujiepusha na uvaaji wa mavazi yasiyo ya heshima mbele ya jamii na kutoa mfano wa vijana wa kiume wanaovaa suruali kwa mtindo wa mlegezo wakiaachia wazi sehemu ya makalio yao na kwamba uvaaji huo unafaa kupigwa vita kwa vile siyo maadili ya watanzania.
 
Naye Ofisa maendeleo ya vijana katika shirika hilo la AGAPE, Helena Daudi aliwataka watoto hao kutokujikatia tamaa ya maisha kwa vile bado wanayo fursa kubwa ya kujiendeleza mara baada ya kuhitimu mafunzo mbalimbali wanayofundishwa hivi sasa ambayo yatawawezesha kujiajiri wao wenyewe baada ya kuhitimu na kujipatia kipato.
 
“Pamoja na kumshukuru mungu kwa kuuona mwaka 2015, niwakumbushe jambo moja muhimu nalo ni kutokukata tamaa ya maisha baada ya kukatishwa masomo yenu kutokana na mimba na wengine wazazi wenu kulazimisha kuolewa kwa nguvu, naamini kupitia fursa hii ya mafunzo mnayopatiwa hapa baadae mtakuwa na matokeo mazuri,” alieleza Helena.
 
Shirika la AGAPE linaendesha mradi wa kupiga vita vitendo vya mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga kwa ufadhili wa Shirika la kimataifa la terre des hommes  la nchini Netherlands ambapo mradi huo umelenga kuwakomboa watoto wa kike zaidi ya 700 waliokatishwa masomo yao  katika wilaya za Kishapu, Shinyanga na Kahama.
 
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top