Picha ya majeraha aliyopata mwananchi aliyeshambuliwa na askari Magereza Shinyanga.

HATIMAYE mkazi wa kijiji cha Nhelegani manispaa ya Shinyanga Lugenzi Maguta (45), aliyeshambuliwa kwa kipigo na askari magereza wa gereza la wilaya ya Shinyanga baada ya kuwanyima soda na biskuti amefikishwa mahakamani na kusomewa shitaka la kufanya fujo gerezani.

Maguta amefikishwa katika mahakama ya mwanzo Shinyanga mjini ambapo upande wa mashitaka ulimsomea shitaka la kuingia gerezani na kufanya fujo akidaiwa kulazimisha kumpatia soda na biskuti ndugu yake aliyekuwa mahabusu shitaka ambalo mshitakiwa amelikana.

Mshitakiwa huyo anashitakiwa kwa kosa la kufanya fujo katika Gereza la wilaya ya Shinyanga mnamo Desemba 7, mwaka jana mnamo saa 5.00 asubuhi alipokuwa amekwenda kumsalimia ndugu yake aliyetajwa kwa jina la Mahushi Nangale aliyekuwa akishitakiwa kwa kosa la kuchukua ng'ombe kutoka kwa baba yake.


Hata hivyo kwa mujibu wa mashitaka aliyosomewa katika mahakama hiyo ya mwanzo ya mjini Shinyanga mbele ya Hakimu Ruth Meshack mshitakiwa huyo alifanya fujo ambazo zingehatarisha usalama wa gereza baada ya kulazimisha kumpatia ndugu yake vyakula (soda na biskuti) ambavyo haviruhusiwa gerezani.

Mara baada ya kusomewa shitaka hilo mshitakiwa alikana kufanya fujo gerezani kama alivyoshitakiwa ambapo hakimu aliuhoji upande wa mashitaka ni njia zipi alizotumia kuingia gerezani mshitakiwa siku hiyo ya tukio iwapo ni za kawaida au alivunja mlango na kujibiwa kuwa aliingia kwa kufuata taratibu zote za magereza.

Mahakama hiyo imeiahirisha kesi hiyo mpaka Desemba 28, mwaka huu itakapoendelea kutajwa mahakamani hapo na mshitakiwa yupo nje kwa dhamana mpaka siku hiyo ya kesi.

Akizungumza nje ya mahakama Maguta aliwaeleza waandishi wa habari kushangazwa kwake na jinsi ambavyo askari magereza waliomshambulia kwa kipigo bila kosa lolote wanavyoshinikiza kutaka kumbambikia kesi japokuwa siku hiyo ya tukio hawakuwa zamu.

Alisema shitaka alilofunguliwa halina ukweli bali chanzo cha  kushambuliwa kwake ni baada ya kuwanyima askari magereza waliokuwa zamu siku hiyo soda na biskuti vyenye thamani ya shilingi 2,000 ambapo wakati akitoka nje ndipo alipodakwa na askari wanaomshitaki hivi sasa waliokuwa wamevaa kiraia waliomrudisha ndani na kuanza kumshambulia kwa kipigo.

“Ninashangazwa na kitendo cha kufunguliwa mashitaka kwamba eti nilifanya fujo gerezani, ajabu watu wanaofungua kesi hii siyo waliokuwa zamu siku hiyo, wao walinihoji eti kwa nini ninawasimulia watu wengine kwamba niliombwa niwachie soda na biskuti askari wenzao waliokuwa zamu siku hiyo baada ya kuelezwa vitu hivyo haviruhusiwi kupewa mahabusu,”

“Sasa kitendo hicho ndicho kilikuwa chanzo cha kushambuliwa kwangu, mmoja wa askari magereza aliyekuwa katika eneo la magereza siku hiyo baada ya kuona nimejeruhiwa miguuni na damu zinanitoka kwa wingi alishauri suala hili tulifikishe kituo cha polisi ili tukalimalizie huko, ajabu kufika wenzangu wakanibambikia kesi ya kufanya fujo,” alieleza.


Hata hivyo kwa upande wake mmoja wa wasemaji wa Jeshi la Magereza mkoani Shinyanga Grace Massawe aliyewahi kuhojiwa na waandishi wa habari juu ya kuwepo kwa tukio hilo alikana kutokea kwa vuguru gerezani ambapo hata hivyo alishangazwa na kitendo cha mwananchi kupigwa akiwa ndani ya gereza kitendo kinachokatazwa hata kama ni kwa mfungwa au mahabusu.



Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top