Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini, Stephen Masele akizungumza na wananchi wa mji wa Shinyanga wakiwemo wanachama wa timu ya Stand United (Chama la Wana). |
TIMU ya Stand United
maarufu kwa jina la “Chama la wana” ya mkoani Shinyanga imepata mfadhili mwingine
mpya atakayeidhamini timu hiyo katika msimu huu wa ligi ya Vodacom kwa shilingi
milioni 100.
Mdhamini huyo ni
Kampuni ya Biko inayoendesha michezo ya kubahatisha kupitia mitandao ya simu hapa
nchini ambayo imefikia makubaliano na timu hiyo inayocheza ligi ya Vodacom
(VPL) kwa kuidhamini kwa kipindi cha msimu mmoja wa 2017/2018.
Akitoa taarifa hiyo
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Shinyanga, mbunge wa Jimbo la
Shinyanga mjini, Stephen Masele alisema kampuni ya Biko imekubali kutoa
udhamini wa shilingi milioni 100 kwa timu hiyo ikiwa ni pamoja na vifaa vya
michezo.
Masele alisema iwapo
Stand United wataonesha mwenendo mzuri kwenye ligi ya mwaka huu, Biko itaongeza
udhamini wake katika msimu ujao wa 2018/2019 kwa kuipatia timu hiyo kiasi cha
shilingi milioni 200.
Hatua hiyo ya kampuni
ya Biko imetajwa itaisaidia zaidi timu ya Stand United ambayo katika msimu
uliopita ilikumbwa na mgogoro mkubwa na kusababisha kumpoteza mdhamini wake aliyekuwa
akiidhamini, kampuni ya Acacia aliyeamua kujitoa.
Kwa upande wake Masele
alisema baada ya timu hiyo kupata viongozi wake waliochaguliwa na wanachama
wenyewe hivi na yeye mwenyewe sasa ameamua kuisimamia kwa ukaribu zaidi ili iweze kufanya vizuri kwenye
ligi ya mwaka huu sambamba na kudhibiti matumizi ya fedha za Klabu.
“Ndugu wanachama na
wapenzi wa timu yetu ya Stand, leo kwetu ni siku ya furaha baada ya kupata
mdhamini mwingine aliyekubali kuidhamini timu yetu kwa kipindi cha mwaka mmoja
huu wa 2017, hii ni baada ya kumpoteza mfadhili wa awali kampuni ya Acacia,”
“Nimezungumza na
wamiliki wa kampuni ya Biko, wamekubali kutushika mkono, na wameahidi tukifanya
vizuri, msimu ujao wa 2018/2019 wataongeza ufadhili wao ambapo utafikia
shilingi milioni 200, na mimi leo nimeamua kujitolea rasmi kuisimamia timu kwa
ukaribu zaidi ili iweze kufanya vizuri,” alieleza Masele.
Masele alifafanua kuwa
katika msimu uliopita aliweza kutafuta wafadhili kampuni ya Acacia waliokubali kuidhamini timu kwa kiasi cha
shilingi bilioni 2.4, lakini baada ya kujitokeza mvutano kati ya pande mbili za
Stand wanachama na Stand Kampuni, Acacia waliamua kujitoa.
Kwa upande wake mwenyekiti
wa Klabu ya Stand United, Dkt. Ellyson Maeja alishukuru mchango wa mbunge
kuwezesha timu hiyo kupata mfadhili mwingine na kwamba kwa upande wao wanachama
na viongozi hivi sasa wana mshikamano mzuri.
“Tunakushukuru sana
mbunge Masele, kwa kweli udhamini huu umekuja kwa wakati muafaka, maana ndiyo
kwanza timu imeanza michezo yake ya ligi, tunaamini zile changamoto tulizonazo
kwa sasa zitapungua kwa kiasi kikubwa, na sisi tunaahidi kuutumia vyema
ufadhili huu wa Biko,” alieleza Dkt. Maeja.
Mbunge Masele na mwenyekiti wa Klabu ya Stand United Shinyanga, Dkt. Maeja. |
Mmoja wa wanachama wa Stand United, Omari Malula akitoa mchango wake wa mawazo wa jinsi ya kuiwezesha timu yao kufanya vizuri katika ligi kuu ya 2017/2018 |
Baadhi ya viongozi na wapenzi wa Timu ya Stand United wakifuatilia hotuba ya mbunge Masele |
Post a Comment