Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Deogratius Mbango akiwa kazini kabla ya kupandishwa cheo.
Deogratius Mbango, askari wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki) ambaye hivi karibuni alitukanwa na mke wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga baada ya kulikamata gari lake kwa kuvunja sheria za barabarani, hatimaye amepandishwa cheo ikiwa ni maagizo ya Rais Dk. John Magufuli.
Askari huyo ambaye alilikamata gari la mke wa waziri huyo baada ya kuvuka sehemu ya waendao kwa miguu eneo la Namanga jijini Dar es Salaam, amepandishwa hatua moja mbele, kutoka koplo hadi sajenti.
Kitendo hicho cha kulikamata gari hilo, bila kujali utambulisho na matusi ya mwanamke aliyedai kuwa mke wa waziri, kilimfanya Rais Magufuli kumsifu na kumuona kuwa jasiri kazini kwake, hivyo kuliagiza jeshi la Polisi kumpa promosheni mara moja.
Juzi Jumapili, gazeti la Uwazi lilimkuta trafiki huyo akiongoza magari maeneo ya Makumbusho katika lango la kuingilia daladala akiwa na cheo kipya cha usajenti.
Alipoulizwa kuhusu kuula huko, Mbango alikiri kutokea kwa jambo hilo na kumshukuru Mungu pamoja na uongozi wa Jeshi la Polisi kwa kumpandisha cheo.
Chanzo: Gazeti la Uwazi.
Post a Comment