Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Gulam Hafidh Muccadam katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mjini eneo la Usia Guest House, akiwa na sehemu ya fedha alizokabidhi kwa vikundi vya vijana na akina mama.

Huyu naye alikuwa miongoni mwa waburudishaji katika mkutano wa mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga.

Mmoja wa wakazi wa Mtaa wa Buzuka akiteta jambo na mburudishaji katika mkutano wa hadhara.


Mwenyekiti wa CCM Tawi la Nkomo, Mzee Ally Maganga akikabidhi sehemu ya msaada wa mmoja wa kiongozi wa kikundi cha wanawake kata ya mjini.


Wakazi wa mtaa wa Buzuka wakifuatilia kwa umakini mkubwa mkutano wa Meya wa Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni diwani wa kata ya Mjini.

HATIMAYE kazi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika barabara za mji wa Shinyanga inatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati ya uongozi wa manispaa ya Shinyanga na watu wa Benki Kuu ya Dunia.

Hali hiyo imebainishwa na Meya ya Manispaa ya Shinyanga, Gulam Hafidh Muccadam alipokuwa akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Usia Guest House mjini Shinyanga ambapo alisema zabuni ya kuwatafuta wakandarasi wa kazi hiyo inatarajiwa kutangazwa mapema mwezi ujao.

Muccadam ambaye pia ni diwani wa Kata ya mjini Shinyanga alisema hivi sasa uongozi wa manispaa hiyo upo katika harakati ya kutekeleza masharti yote muhimu yaliyotolewa na watu wa benki ya dunia ikiwemo kutenga fedha zinazohitajika kuchangwa na manispaa ili msaada huo uweze kutolewa.

Mbali ya taarifa hiyo pia Meya huyo alisema upo uwezekano wa vijana wa Shinyanga kupata nafasi ya masomo katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Sudan ambapo serikali ya nchi hiyo imekubali kutoa nafasi kadhaa  zitakazowezesha wanafunzi watakaofaulu vizuri mitihani ya kumaliza kidato cha sita waweze kwenda kusoma katika nchi hiyo.

“Wakazi wa Shinyanga tuna kila sababu ya kuongeza ushirikiano wetu katika shughuli za kimaendeleo, tuache kukaa tukipigana majungu, kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wangu yapo mambo mengi nimefanya, lakini kwa leo nipende kuwafahamisha tu kazi ya ujenzi wa barabara zetu kwa kiwango cha lami tayari iko mbioni kuanza,”

“Katika zunguka zunguka yangu pia nimekubaliwa kupewa nafasi kadhaa katika vyuo vikuu nchini Sudan ambako vijana wetu watakaohitimu vizuri masomo yao ya kidato cha sita watakwenda kusoma kwa ufadhili wa nchi hiyo, sasa ni juu ya watoto wetu kuongeza bidii katika masomo yao ili waweze kuitumia fursa hii,” alieleza Muccadam.

Meya huyo alisema mbali ya fursa ya nafasi ya vyuo vikuu lakini pia nchi ya Sudan imekubali kuleta madaktari bingwa wa macho katika mji wa Shinyanga ambao watakaotoa huduma ya matibabu bure kwa watu wenye matatizo mbalimbali ya macho ikiwemo kufanya upasuaji na kugawa miwani ya kusomea na kuonea ipatayo 1,500.

Katika hatua nyingine meya huyo alitoa msaada wa zaidi ya shilingi milioni nane kwa vikundi vinane vya vijana na wanawake ikiwemo vyerehani vinane ili waweze kujianzishia shughuli za uzalishaji mali ambapo kila kikundi kilikabidhiwa fedha taslimu shilingi 300,000.

“Ndugu zangu wa kata ya mjini nilipokuwa nikiomba kura kwenu nilisema iwapo mwenyezi mungu akinipa uwezo, nitawawezesha, na sasa amenipa uwezo huo nimeona nianze kuwawezesha, nataka vijana na akinamama wa kata ya mjini mfanye kazi, mbali ya shilingi 300,000 kwa vikundi vinane lakini pia ninawapa shilingi 500,000 kila kundi shilingi 250,000,”

“Hizi 500,000 ni mtaji, vijana shilingi 250,000 na wanawake 250,000 mkanunulie majora ya vitambaa tayari kwa kuanza kazi za ushonaji, nimekupangishieni na vyumba ambavyo nimelipia kodi ya mwaka mzima, kazi kwenu, kafanyeni kazi, acheni kushinda vijiweni bila kazi, na ninaahidi kufanya zaidi kadri mungu atakavyoniwezesha,” alisema Muccadam.

Muccadam aliwaomba wakazi wa kata yake ambao bado hawajaanzisha vikundi vya uzalishaji mali waweze kuanzisha vikundi hivyo ili waweze kusaidiwa kwa kupatiwa fedha ya kuendeshea vikundi hivyo.



Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top